Wananchi wa Sudan waendelea kusubiri serikali mpya baada ya Bashir

Waziri Mkuu wa mpito wa Sudani Abdallah Hamdok wakati wa shereheya kuapishwa kwake, Khartoum Agosti 21, 2019.

Nipashe Online: Waziri Mkuu wa Sudani Abdallah Hamdok amechelewesha kutangazwa kwa serikali ya kwanza nchini Sudani tangu rais Omar al-Bashir kutimuliwa madarakani, ili kuweza kuendelea na majadiliano kuhusu uteuzi wa mawaziri wake, amesema afisa mmoja nchini Sudani.

Serikali hii mpya inatarajiwa kukabiliwa na changamoto kubwa baada ya miongo mitatu ya utawala wa kijeshi na miezi kadhaa ya maandamano yaliyopelekea jeshi kumtimua na kumkamata aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir.

Kulingana na makubaliano ya kihistoria yaliyosainiwa Agosti 17 kati ya viongozi wa waandamanaji na wanajeshi, serikali mpya ilitarajiwa kutangazwa Jumatano wiki hii.

Lakini tangazo hilo lilicheleweshwa kwa sababu “majadiliano juu ya uteuzi wa mawaziri bado yanaendelea,” kilisema chanzo kilio karibu na Hamdok, aliyetawazwa Agosti 21. Chanzo hiki hakijabainisha ni lini serikali mpya itatangazwa.

Waziri mkuu anatarajia kuteua wajumbe wa baraza lake la mawaziri kati ya majina yaliyopendekezwa na vuguvugu la Uhuru na Mabadiliko (FLC), kundi la wanarakati walioanzisha maandamano nchini Sudani.