Vyama vikuu vya Israel vyaanza mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano

Nipashe Online: Vyama viwili vikuu vya Israel vinakutana leo kuanza mazungumzo ya uwezekano wa kuunda serikali ya muungano kati yao.

Hii ni baada ya mkwamo kwenye matokeo ya uchaguzi mkuu uliorudiwa wiki iliyopita, ambapo hakuna chama kilichopata wingi unaohitajika ili kuweza kuunda serikali.

Mkutano wa leo kati ya vyama hivyo, unajiri siku moja tu baada ya kiongozi wa chama chaSamawati na Nyeupe Benny Gantz pamoja na waziri mkuu Benjamin Netanyahu anayekiongoza chama Liqud, kukutana kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi huo ulipofanyika.

Rais wa Israel Reuven Rivin aliwaleta Netanyahu na Gantz pamoja kwa matumaini ya kuvunja mkwamo uliopo unaoweza kuiweka nchi hiyo katika hali ya sintofahamu na pia unaweza kulazimisha uchaguzi mwingine wa tatu kufanywa chini ya muda wa mwaka mmoja.

Rais wa Israel ana wajibu wa kumchagua mmoja miongoni mwa washindani kuwa waziri mkuu baada ya uchaguzi.