Teknolojia inayowatambua wapenzi wa jinsia moja

Utafiti ambao unafanyia majaribio teknolojia inayodaiwa kuwa na uwezo wa kutofautisha watu wapenzi wa kawaida na wapenzi wa jinsia moja umezua mzozo mkali kati ya waliotayarisha teknolojia hiyo na watetezi wa haki za wapenzi wa jinsia moja.

Watafiti hao kutoka Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani wanadai kwamba wameunda programu ya kompyuta ambayo inaweza kuangalia uso wa mtu na maumbile yake na kutofautisha kati ya wapenzi wa jinsia moja na wapenzi wengine.

Programu hiyo inaweza kutambua mambo ambayo mtu wa kawaida hawezi kuyabaini, wanasema.

Lakini watetezi wa haki za mashoga wameshutumu utafiti huo na kusema ni “hatari” na “sayansi isiyo na manufaa”.

Lakini wanasayansi wanaohusika wamesema wanaopinga programu hiyo hawajaielewa vyema.

Maelezo ya kina kuhusu mradi huo yatachapishwa katika jarida moja kuhusu sifa za watu na saikolojia ya kijamii.

Katika utafiti huo, wataalamu waliunda programu kwa kutumia picha za wanaume 14,000 wazungu kutoka kwa tovuti ya kutafuta wapenzi.

Walitumia picha kati ya moja na tano za kila mtu na kurekodi msimamo wa mtu kimapenzi kama alivyojitangaza katika tovuti hiyo ya kuchumbiana.

Wataalamu hao wanasema programu waliyoiunda ilionekana kuwa na uwezo wa kuwatofautisha wanaume na wanawake wapenzi wa kawaida na wapenzi wa jinsia moja.