Taifa Stars wajinoa makali kuwakabili Sudan

Nipashe Online: Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” inaendelea na kambi yake ya kujiwinda dhidi ya Sudan mchezo wa kufuzu hatua ya makundi ya mashindano ya Chan yakayofanyika mwaka 2020 nchini Cameroon kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani.

Ikiwa maandalizi hayo yanaendelea kaimu kocha msaidizi wa kikosi cha Stars Juma Mgunda amejinasibu kuwa timu ya taifa iko katika hali nzuri na ipo tayari kupambania ushindi.

Mgunda ambaye mbali na majukumu ya Kitaifa pia ni kocha mkuu wa klabu ya Coastal Union ya Tanga inayoshiriki Ligi Kuu bara.

Akizungumza kuelekea mtanange huo, Mgunda amesema kuwa wachezaji wanatambua kazi yao kubwa ni kutafuta matokeo na wapo tayari kwa hilo.

“Mapungufu ambayo yalikuwepo awali hasa kwenye safu ya ushambuliaji ndiyo tunayafanyia kazi kwa ukaribu kwani ili timu ishinde ni lazima ipate mabao mengi kwa kuwa tunaanza nyumbani basi tunapambana kupata matokeo chanya,” amesema.

Tanzania itapepetana vikali na Sudan siku ya Jumapili Septemba 22 katika dimba la Mkapa Jijini Dar es Salaam kabla ya kurejea wiki moja baadae.

Itakumbukwa safari ya Tanzania kwenye michuano hii ilianzia kwa kuitoa Kenya “Harambee Stars”.