Rais wa zamani wa Ufaransa Jacques Chirac afariki dunia

Nipashe Online: Rais wa zamani wa Urafansa Jacques Chirac amefariki dunia.

Familia yake imesema rais huyo wa zamani wa Ufaransa amekufa kwa amani akiwa na umri wa miaka 86.

Rais wa zamani wa Ufaransa, mwanasiasa aliyefuata siasa za mrengo wa wastani zinazoengemea kulia,aliiongoza Ufaransa kati ya mwaka 1995 na 2007, ameaga dunia Alhamisi (26.09.2019) akiwa na umri wa miaka 86.

Mwanasiasa huyo mkongwe amekufa leo kwa amani asubuhi akiwa amezungukwa na watu wa familia yake,  mkwe wake Frederic Salat-Baroux aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP. Hata hiyo hakueleza sababu ya kifo chake.

Chirac alihudumu kama meya wa jiji la Paris na aliwahi kuwa waziri mkuu mara mbili kabla kuwa rais mwaka 1995 hadi 2007.

Hali yake ya afya ilidhoofika tangu alipopatwa na kiarusi mwaka 2005 alipokuwa madarakani.