Mwanamume asulubiwa Uganda kwa kuunga mkono chama tawala

Nipashe Online: Polisi nchini Uganda inachunguza kisa ambapo mwanamume mmoja ameshambuliwa na kujeruhiwa vibaya kwa madai ya kuunga mkono chama tawala cha National Resistance Movement (NRM).

Baker Kasumba, anayesadikiwa kuwa na umri wa chini ya miaka 21 aliripotiwa kushambuliwa na watu wawili wasio julikana akitoka kazini kuelekea nyumbani katika eneo la Kalerwe siku ya Alhamisi.

Gazeti la Daily Monitor nchini Uganda limeripoti kuwa taarifa iliondikishwa na muathiriwa katika kituo cha polisi cha Kalerwe, inasema Kasumba alidai alishikwa kupigiliwa misumaru kwa nyundo na watu ambao hakuwafahamu kwa kuvalia kofia ya NRM ambayo huvaliwa na wanaharakati wa chama tawala.

Kulingana na taarifa hiyo maafisa wanasema muathiriwa alifungwa mikono pamoja alafu akawekewa kofia hiyo katikati ya mikono yake na kupigiliwa misumari kwa kutumia nyundo.

Bw pia ameripotiwa kueleza polisi kuwa waliomshambulia walimwambia tunakusulubisha ili ufariki kwa ajili ya chama anachokienzi

Naibu msemaji wa polisi mjini Kampala Luke Owoyesigyire, amesema kuwa polisi ameanzisha msako mkali kuwatafuta washukiwa.

Kisa hicho kimepokelewaje?

Kisa hicho kimezua gumzo kali katika mitandao ya kijamii huku baadhi ya wafuasi wa upinzani wakidai kuwa ni njama ya serikali.

Kashari Boy aliandika katika Twiiter yake akisema mhalifu ni mhalifu haijalisha anaunga mkono chama gani cha kisiasa.

Judith Kukundakwe Asiimwe anadai kuwa hatua hiyo ni njama ya inayo endeshwa na kikosi maalum cha usalama kinachofahamika ili ”kuchafua sifa ya vijana wa People Power”.

”Nina ushahidi wa kutosha kuthibitisha hilo” aliandika Asiimwe katika Twitter yake .

Naye Roxanne Daphne aliandika ”Hili ni kosa kubwa sana, sote tuna uhuru wa kuwa na maoni yetu ya kisiasa”aliandika.

Kasumba anasemekana kuokolewa na wanawake wawili walioshuhudia tukio hilo na kupiga mayowe hatua ambayo iliwafanya washukiwa kutoroka.

Kulingana na taarifa yake kwa polisi muathiriwa alisema siku chache zilizopita alionywa na mfanyikazi mwenzake kutomuunga mkono rais Museveni na chama chake na kuongeza kuwa huenda alipanga watu kumvamia.

Tukio hilo la kushangaza kwa mujibu wa Daily Monitor lilitokea karibu mita 30 kutoka kituo cha polisi cha Kibe.

Baker Kasumba anaendelea kupokea matibabu katika hospitali kuu ya Mulago baada ya kuondolewa na polisi katika eneo la shambulio.