Mwanamke aliyekuwa amekaribia kujifungua ajiua China

Mitandao ya kijamii nchini China inajibu kwa mshangao na kutamaushwa, baada ya mwanamke mmoja aliyekuwa mjamzito kujiua kutokana na madai kuwa familia yake ilikataa kumruhusu ajifungue kwa njia ya upasuaji.

Mwanamke huyo wa umri wa miaka 26, aliruka kutoka dirisha la hospitali katika mkoa wa Shaanxi tarehe 31 mwezi Agosti. Mtoto ambaye alikuwa amebebwa na mwawamke huyo naye alifariki.

Huo Junwei, daktari katika hospitali ya Yulin Number One hospital, aliambia gazeti la China Economic Daily, kuwa Bi Ma alitoka nje ya chumba cha wagonjwa mara mbili na kuiambia familia yake kuwa alikuwa akipitia machungu makali, na kuwa alikuwa akitaka afanyiwe upasuaji lakini familia ilikataa kumrusu afanyiwe hivyo.

Hata hivyo mume wa Yana anakana na kuliambia gazeti la Beijing Youth Daily kuwa, “hatukukosa kukubaliana kuhusu njia ya upasuaji”.

Taarifa kutoka hospitalini zinasema kuwa Bi Ma, alikuwa na mimba ya wiki 42 na kwamba, madakatari walikuwa wameamua kuwa kutokana kichwa cha mtoto kuwa kikubwa, kujifungua kwa njia ya kawaida ingekuwa hatari.

Hospitali ilisema kuwa waliomba ushauri wa “familia ilisema kuwa ilielewa na ikakataa afanyiwe upasuaji”.