Man City wana ‘kikosi ghali zaidi katika’ soka duniani

Manchester City ndiyo klabu iliyo na wachezaji ghali zaidi duniani kwa pamoja, kwa mujibu wa utafiti wa shirika la CIES Football Observatory.

City walitumia £215m dirisha la kuhama wachezaji katika majira ya joto na kufikisha jumla ya gharama ya kikosi chao hadi euro 853m (£775m).

Thamani hiyo ni £3m zaidi ya pesa zilizotumiwa na Paris St-Germain, waliomnunua Neymar majira ya joto kwa rekodi ya dunia ya £200m.

Manchester United, ambao wametumia euro 784m (£712m) kuunda kikosi chao cha sasa, wanashikilia nafasi ya tatu.

Walikuwa wanaongoza mwaka uliopita, lakini thamani ya kikosi chao ilipanda kwa £66m pekee majira ya joto.

Takwimu za CIES zinaangazia ligi tano kuu za Ulaya – ligi kuu za England, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uhispania.

Klabu za Ligi ya Premia zinajaza nafasi sita kati ya nafasi kumi za juu, ambapo vikosi vyake vina thamani ya wastani ya euro 287m (£261m).