Magufuli: Rushwa, udanganyifu bado changamoto Tanzania

Nipashe Online: Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema rushwa zinazotozwa na maafisa wa serikali na udanganyifu unaofanywa na wafanyabiashara ni baadhi ya vikwazo vikubwa vinavyoandama ukuaji wa biashara na uchumi nchini Tanzania.

Akizungumza katika mkutano maalum alioutishaleo na wafanyabiashara zaidi ya 1,000 kutoka kila kona ya Tanzania Magufuli amesema japo kuna jitihada kubwa zinazofanyika kupambana na rushwa, bado kuna maafisa wa serikali si waaminifu.

Magufuli ameyataja maeneo yanayoongoza kwa rushwa ni bandarini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), barabarani pamoja na mipakani.

“Jitihada kupambana na rushwa zinaendelea…kuna mfanyabiashara alishawahi kusema kuwa ukitaka kuona rushwa bado ipo, toa kontena bandarini hadi Kariakoo. Sijui kama tumeshafanyia kazi kauli ile…” amesema Magufuli.

Magufuli toka alipoingia madarakani amekuwa akijipambanua kwa kuchukia rushwa na kuahidi kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo hilo.

Vigogo kadhaa wa serikali wamefutwa kazi na baadhi yao pamoja na wafanyabiashara wakubwa wamefunguliwa mashtaka mbali mbali ya ufisadi.

Hii leo, amewaasa wafanyabiashara kwenye mkutano huo wasisite kuwaripoti maafisa wanaowaomba rushwa kwa mamlaka ili wachukuliwe hatua.

Magufuli pia amekiri kuwa bado serikali haijaweka mipango endelevu ya kuwaendeleza wafanyabiashara na sekta binafsi kwa ujumla wake ili wachangie zaidi kwenye kuujena uchumi wa nchi yao.

“Hapa kwetu tuna zaidi ya wajasiriamali milioni lakini tumeshindwa kuwa na mipango ya kuwatambua, kuwalinda na kuwaongozea tija,” amesema na kuongeza: ” Mpaka sasa ni watu milioni 2.7 pekee ambao ndio wanaolipa kodi. Wigo kati ya wanaolipa na wasiolipa kodi ni kubwa sana, njia moja ya uhakika ya kutatua hili ni mipango thabiti ya kurasimisha wajasiriamal ili waendeshe uchumi.”

Magufuli pia ametaja utitiri wa kodi na taasisi za udhibiti kama ni chamgamoto nyengine ya kimfumo inayoathiri ukuaji wa biashara nchini Tanzania. Lakini amesema jitihada za kutatua changamoto hiyo zinafanyiwa kazi na wameanza kwa kufuta tozo a ada zaidi ya 100 kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

Kwa upande wa wafanyabiashara, Magufuli amesema wapo ambao si waaminifu wanakwepa kodi kwa kutoa rushwa na wengine kufanya udalali na kujihusisha na makundi ya uhalifu wa kibiashara.

Magenge hayo ya kihalifu wa kibiashara amesema yapo katika biashara ya sukari, mafuta ya kula na korosho.

“Baadhi yao wamekuwa wakitumia mbinu ya kukwepa kodi kwa kudai marejesho ya fedha ya ongezeko la thamani (VAT) wakati mauzo yaliyofanyika ni hewa ya biashara za nje na kwenye hili nataka niseme wazi nina orodha ya kampuni 17,446 ambazo zimehusika na tuhuma hizo.

“Nitawapa copy (nakala) ya kampuni hizo hewa ili mkafanye uchambuzi wenu na kama yalikwepa kitu chochote yakajipange kulipa ndani ya siku 30,” amesema Rais Magufuli.

Suala la marejesho ya pesa ya makusanyo ya VAT limekuwa kubwa na kugusiwa katika ripoti ya hivi karibuni ya Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) ambao wanasema marejesho ambayo hayajafanywa na serikali ni kiasi cha Tsh 2.3 trilioni (takriban dola bilioni 1) kwa kipindi cha miaka 2-3 iliyopita.

Rais Magufuli hata hivyo amesema moja ya sababu ya suala hilo kuwa kubwa ni udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara.

“…kumekuwa na uongezaji wa marejesho ya fedha ya VAT kwa wafanyabiashara ili waweze kupewa fedha nyingi kutoka serikalini huu ni wizi.”

Tatizo jengine la wafanyabiashara lilogusiwa na Magufuli ni kubadli matumizi ama kutoendeleza kabisa viwanda ama ardhi walizobinafsishiwa na serikali bila kufuata utaratibu.

“Wengine wametumia maeneo hayo kukopa fedha benki kwa ajili ya kazi hiyo na hawajafanya, hiyo ni dhambi na wengine najua mko hapa.”

“Baadhi ya wafanyabiashara wamejanga viwanda kama gelesha na kuvitumia kupokea bidhaa kutoka nje bila kulipa kodi stahiki kama vile bidhaa hizo zimetengenezwa nchini.” amesema