Korea Kaskazini yafyatua makombora kuelekea Japan

Nipashe Online: Korea Kaskazini imefyatua makombora ambayo hayajatambuliwa mara moja kuelekea Bahari ya Mashariki, ambayo pia hujulikana kama Bahari ya Japan.

Taarifa hizi ni kulingana na shirika la habari la Korea Kusini la Yonhap, lililonukuu muungano wa wanadhimu wakuu wa jeshi, JCS.

Kulingana na JCS, makombora hayo yalifyatuliwa kutokea mji wa bandari wa Korea Kaskazini, Wonsan.

Muda mfupi baadae, msemaji wa serikali ya Japan Yoshihide Suga ilisema kombora moja limeangukia kwenye maji ya ukanda maalumu na huru wa kibiashara wa Japan.

Waziri mkuu Shinzo Abe amelaani hatua hiyo na kuagiza kufanyika uchunguzi.

Tukio hili, linafuatia tangazo lililotolewa na Washington na Pyongyang hapo jana la mazungumzo kuhusu mipango ya nyuklia ya Korea Kaskazini wiki ijayo, baada ya yale ya Februari kumalizika bila ya makubaliano.