Kipande kikubwa cha barafu chameguka Antarctica

Kipande kikubwa zaidi cha barafu kuwahi kuonekana duniani kimemefuka kutoka kwenye eneo la Antarctica.

Jiwe hilo kubwa la barafu linakadiriwa kuwa na ukubwa wa kilomita mraba 6,000, ukubwa sawa na wa eneo la Wales nchini Uingereza.

Kipande hicho cha barafu kina ukubwa mara 50 kushinda kisiwa cha Manhattan, Marekani

Satelaiti ya Marekani ilionesha jiwe hilo kubwa likiwa limemeguka ilipokuwa inapitia eneo la barafu lifahamikalo kama Larsen C Jumatano.

Wanasayansi walikuwa wanatarajia hilo. Wamekuwa wakifuatilia ufa mkubwa katika barafu ya Larsen kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Larsen C ndiyo sehemu kubwa ya barafu iliyo kaskazini zaidi mwa dunia eneo la Antarctica.

Watafiti walikuwa awali wamesema iwapo eneo hilo lingepoteza kipande hicho cha barafu basi sehemu yote yenyewe itakuwa hatarini ya kupasuka tena siku za usoni.

Eneo la barafu la Larsen C lina kina cha mita 350.

Barafu hiyo huelea maeneo ya pembeni Antarctica Magharibi na kuzuia mito ya barafu ambayo huisaidia kukaa imara.