Jeshi la Uganda lapiga marufuku Baret nyekundu ya Peoples power

Jeshi la uganda UPDF limefanya mabadiliko katika sare zake za kijeshi katika vikosi mbali mbali na kutangaza katika gazeti rasmi la serikali.

Hii ni baada ya kuidhinishwa tarehe 18 mwezi huu wa Septemba na baraza la kijeshi.

Kwa mujibu wa sheria hiyo mtu yoyote atakayevaa sare za jeshi atafunguliwa mashitaka katika mahakama ya kijeshi.

Wanasiasa wa upinzani nchini Uganda chini ya vugu vugu la Peoples Power linaloongozwa na mbunge msaanii Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine,hata hivyo wameapa kuendelea kuvaa mavazi ya vugu vugu lao, licha ya jeshi la UPDF kutangaza mavazi yao mapya ikiwa na kofia inafanana na ya Peopes Power.

Mwanasiasa wa upinzani na msanii Bobi Wine, amekua akivalia kofia nyekundu kama ”nembo ya uasi”.

Mwanasiasa na msanii wa Uganda Bobi WineHaki miliki ya picha GETTY IMAGES

Japo Bobi Wine hajatoa tamko lolote kuhusiana na sheria hiyo mpya lakini baadhi ya viongozi wa waandamizi wa vugu vugu la People Power wameliambia shirika la habari la AFP kwamba wataendelea kuvaa kofia hiyo.

“Tutaendelea kuvaa kofia zetu nyekundu,” alisema kiongozi wa vijana Ivan Boowe. “Hakuna mtu atakayetutisha wala kututia uoga kwa kupigania haki yetu.”

“Kwa kujumuisha kofia yetu katika sare za kijeshi, serikali inapanga njama ya kupiga marufuku vugu vugu la People Power na tuko tayari kukabiliana na hatua itakayotekelezwa na serikali,”aliongeza.

Naibu wa msemaji wa jeshi la UPDF luteni kanali Deo Hakik ameifahamisha BBC kuhusu sare azao mpya na kukosoa wale wote wanaozitumia.

”Kitu ambacho tulikua tunaomba au tumeweka kwenye sheria kimeshatengenezwa na kwa sasa hivi UPDF iko na mavazi ambayo inajulikana na ambayo iko kwa sheria na hatujatoa mavazi hayo jana”

Luteni kanali Hakik ameongeza kama kuna mtu fulani aliyetengeneza mavazi yake bila kuzingatia sheria hiyo sio shida yao akisisitiza kuwa hawatengenezi mavazi yao kwa kufuatilia mambo ya siasa au biashara.

” Uganda imekua na shida mingi sana kuona kwamba waraia au wajambazi wanavalishwa mavazi yetu kufanyamadhambi’ na watu huko nje wanafikiri UPDF ndio wanafanya madhambi fulani” alisema.

Lakini mwanasheria wa vugu vugu la Peoples power ambaye pia ni mbunge wa upinzani Asumani Vasalirwa ameifahamisha BBC kuwa wataendelea kuvaa bareti zao.

”Kofia ya jeshi ina muonekano tofauti inayoitambulisha kama kofia ya jeshi sasa kofia ya People powe haifananani na hiyo ya kijeshi”

Pia ameongeza kwamba mavazi hayo mapya yanalenga vuugu vugu lao kwa lengo la kudhoofisha harakati zao za kupigania haki kwani wamepata ufuasi mkubwa.

”Vijana kila mtu anavaa kofia iko na impact kubwa kwa wananchi sasa tunafikiri chama cha NRM kinataka kutukandamiza kupita kwa jeshi watoe sheria watu waogope”

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema hatua hiyo ni njama ya kupunguza makali ya vuguvugu la Peoples Power wakati ambapo Uganda inajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.

Tayari kiongozi wa vugu vugu hilo Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine ametangaza kugombea kiti cha urais dhidi ya Rais Yoweri Museveni ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 30.