Iran yatoa onyo kali kwa Marekani

Nipashe Online: Iran kupitia jenerali wa kikosi cha kimapinduzi imeonya kwa kusema nchi yoyote itakayoanzisha vita dhidi yake,ardhi ya nchi hiyo itageuka kuwa uwanja wa vita vikubwa.

Kamanda wa kikosi cha walinzi wa kimapinduzi nchini Iran ameonya Jumamosi kwamba nchi yoyote itakayoishambulia jamhuri hiyo ya kiislamu itashuhudia ardhi yake ikigeuka kuwa uwanja mkuu wa vita. Meja Jenerali Hossein Salami ametowa onyo hilo wakati akifunguwa maonyesho ya ndege zisizokuwa na rubani zilizokamatwa na Iran.

Kamanda huyo amesema Iran iko tayari kukabiliana na tukio lolote,katika wakati ambapo kuna ripoti kwamba Marekani inapima hatua za kijeshi itakazochukuwa kujibu mashambulizi yaliyofanywa hivi karibuni dhidi ya visima vya mafuta vya Saudi Arabia,mashambulizi ambayo yanadaiwa yalifanywa na Iran.

Salami ameuambia mkutano wa waandishi habari mjini Tehran kwamba yoyote anayetaka kuona nchi yake inageuka kuwa uwanja mkuu wa vita basi anaweza kuendelea na mpango wa kuishambulia Iran.

Kadhalika amesema hawatokubali kuruhusu vita vya aina yoyote viingie katika ardhi ya Iran na ni matarajio yao kwamba Marekani haitofanya kosa la kimkakati kama ilivyowahi kufanya huko nyuma.

Kamanda huyo wa kikosi cha ulinzi cha kimapinduzi cha Iran ameyazungumza haya akiwa katika jumba la makumbusho ya mapinduzi ya kiislamu na ulinzi wakati wa kufunguliwa kwa maonesho ya kile kinachoitwa na Iran kuwa ni ndege zisizokuwa na rubani za Marekani na nchi nyingine zilizokamatwa katika ardhi yake.

Katika maonesho hayo walinzi wa Kikosi cha kimapinduzi pia walionesha silaha za ulinzi wa anga zilizotengenezwa nchini humo ambazo ni bateri aina ya  Khordad 3,ambazo ziliwahi kutumika kudungua ndege isiyokuwa na rubani ya kivita ya Marekani mnamo Juni 20. Jenerali Salami amesema Iran imeshaizima katika kuhodhi teknolojia kwenye ulinzi wa anga na utengenezaji wa ndege zisizokuwa na rubani.

Amehoji jenerali huyo ,ndege zisizokuwa na rubani za Marekani zinafanya nini kwenye anga ya Iran?na kuongeza kwamba wataziangusha na kulenge kitu chochote kitakachoingia kwenye anga ya Iran. Onyo hili kali la Iran linakuja siku chache tu baada ya kushambuliwa visima vya mafuta vya Saudi Arabia ambapo kundi la waasi wakihouthi nchini Yemen wamedai kuhusika.

Marekani lakini imekata kauli kwamba mashambulio hayo yalifanywa kwa kutumika makombora yenye uwezo na kasi kubwa aina ya Cruise  kutoka Iran na kukitaja kitendo hicho kuwa cha kivita.

Saudi Arabia yenyewe ambayo imejitumbukiza kwenye vita vya miaka mitano  nchini Yemen, imesema hakuna mjadala kwamba Iran imefadhili mashambulizi hayo na silaha zilizotumiwa zimetengezwa ndani ya Iran lakini haijasema kwamba hasimu wake huyo katika kanda hiyo inahusika moja kwa moja.

Na kutokana na hali iliyopo jenerali Salami pia amesikika akisema kwamba wakati mwingine Marekani inazungumzia kuhusu kuchukua hatua za kijesho lakini matumizi ya nguvu za kijeshi kwa muda, hayawezi kubakia kwa kipindi kifupi kwasababu Iran imeshajitolea kujibu na itafanya hivyo bila ya kupumzika hadi pale wenye mabavu watakapoporomoka.