Iran yaionya Marekani juu ya vita vya kiuchumi

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif

Nipashe Online: Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Mohamed Javad Zarif, leo ameionya Marekani kuwa haitokuwa salama baada ya kuanzisha kile alichokiita vita ya kiuchumi dhidi ya Iran.

Akionekana mwenye ghadabu, Zarif ametoa mfululizo wa vitisho dhidi ya Marekani wakati wa ziara ya waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Heiko Maas, mjini Tehran anayejaribu kupunguza mvutano unaoongezeka katika eneo la Ghuba.

Zarif amesema njia pekee ya kutuliza hali ya wasiwasi iliyopo ni kwa kuondoa vita ya kiuchumi dhidi ya Iran na kuongeza yule aliyeanzisha vita hivyo dhidi Iran hatoweza kuvimaliza.

Chanzo cha mvutano uliopo ni uamuzi wa Marekani wa kujitoa kutoka mkataba wa nyuklia na Iran na kuongeza vikwazo vya kuchumi dhidi ya taifa hilo la Ghuba ya Uajemi.

Kwa upande wake, Maas amesisitiza kuwa Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya yanataka kutafuta njia ya kuyanusuru makubaliano ya nyuklia ambayo yameshuhudia Iran ikipunguza urutubishaji madini ya Urani ili iondolewe vikwazo vya uchumi.