Huawei yalalamikia kuzuiwa soko la Marekani

Nipashe Online: Kampuni kubwa ya mawasiliano ya Huawei ya nchini China, imelalamikia ilichokiita ”vizuizi visivyo na msingi” kwenye soko la Marekani, baada ya Rais Donald Trump kutangaza hali ya dharura ya kulinda mitandao ya mawasialiano ya Kimarekani.

Katika hali hiyo, serikali ya Marekani inayo mamlaka ya kupiga marufuku teknolojia ya makampuni kutoka ”mahasimu ya nje” ambayo yanaweza kuwa kitisho kwa usalama wa taifa.

Kampuni ya Huawei na wawakilishi wake wamewekwa kwenye orodha inayohitaji ridhaa ya serikali mjini Washington, kuweza kununua teknolojia ya kimarekani.

Huawei imesemaa iko tayari kuzungumza na Marekani kuhusu njia zenye tija za kuhakikisha kuwa bidhaa zake zinakidhi vigezo vya kiusalama.

Kampuni hiyo imeonya kuwa kuizuia kwenye soko la Marekani hakutaifanya nchi hiyo kuwa salama zaidi, bali kutawalazimisha wanunuzi nchini humo kupata bidhaa hafifu za kiteknolojia tena kwa bei kubwa.