Dawa ”tamu” ya mbu iliofanikiwa Tanzania

Je wajua kwamba mbu huvutiwa na vitu vitamu?.

Hivyobasi wanasayansi wametumia fursa hiyo kutengeza dawa iliochanganywa na sukari ili kuwavutia kwa lengo la kuwaua.

Dawa hiyo imechanganywa na kemikali iliowekwa harufu ya sukari inayoweza kuwavutia wadudu hao .

Imegunduliwa kuweza kuangamiza mbu katika vijiji vya Tanzania vyenye ugonjwa mwingi wa malaria ambapo majaribio yamefanywa.

Dawa hiyo kwa jina Vectrax inaweza kupiga jeki juhudi za kupunguza malaria, Zika na magonjwa mengine yanayosababishwa na mbu duniani.

Mwanasayansi wa Brazil aliyenzisha dawa hiyo Agenor Mafra Neto anasema kuwa lengo lake ni kuifanya kuwa ya bei rahisi na kuhakikisha kuwa imesambazwa kupitia Umoja wa Mataifa na mashirika yasiokuwa ya kiserikali.

“Mchanganyiko wa kemikali tunayotumia kuwavutia mbu una nguvu mno hatua ambayo inawafanya kutovutiwa na harufu nyengine za mimea ya kawaida”, alisema Agenor.

Anasema kuwa ni sawa na kuwa na duka la chocolate katika kila pembe.

Bidhaa hiyo ni kivutio kikubwa hatua inayowafanya kuila licha ya kuwa na kemikali za dawa ya wadudu.

Mbali na hilo mabaki ya dawa hiyo yanaweza kuchafua udongo na kuukinga dhidi ya wadudu.