Bomu la USSR lililoishangaza dunia

Mapema asubuhi, mnamo 30 Oktoba 1961, ndege ya kuangusha mabomu ya Muungano wa Usovieti aina ya Tu-95 ilipaa kutoka uwanja wa kambi ya ndege za kivita ya Olenya katika rasi ya Kola kaskazini mwa Urusi.

Tu-95 ilikuwa ndege kubwa sana yenye injini nne ambayo iliundwa mahsusi kubeba mabomu.

Katika mwongo mmoja uliotangulia, Muungano wa Usovieti ulikuwa umepiga hatua sana katika utafiti kuhusu nyuklia.

Marekani na USSR zilikuwa zimejipata upande mmoja wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia lakini baada ya vita, kukatokea Vita Baridi.

Wasovieti baada ya kujipata wanakabiliwa na taifa pekee lililokuwa na silaha za nyuklia, iliona njia pekee ya kushindana vyema na Marekani ilikuwa ni kuwa na silaha zake za aina hiyo.

Tarehe 29 Agosti 1949, Wasovieti walikuwa wamefanyia majaribio silaha yake ya kwanza ya nyuklia kwa jina ‘Joe-1’ katika eneo ambalo sasa linapatikana Kazakhstan.

Walitumia ujuzi uliopatikana kwa kuingia kisiri na kupata taarifa kuhusu mpango wa atomiki wa Marekani.

Katika miaka iliyofuata walikuwa wamepiga hatia sana. Walikuwa wamelipua silaha zaidi ya 80 za atomiki kipindi hicho. Mwaka 1958 pekee, Wasovieti walikuwa wamefanyia majaribio mabomu 36 ya nyuklia.

Lakini hakuna bomu hata moja walilokuwa wamefanyia majaribio awali ambalo lilikaribia bomu lililokuwa limebebewa na ndege hiyo aina ya Tu-95.

Lilikuwa bomu kubwa sana, bomu ambalo halingetoshea sehemu ya kubebea mabomu ya ndege.

Bomu hilo lilikuwa na urefu wa 8m (26ft), kipenyo cha karibu 2.6m (7ft) na lilikuwa na uzali wa tani 27.

Muonekano wake ulikuwa sawa na mabomu yaliyopewa majina ‘Little Boy’ na ‘Fat Man’ ambayo yalikuwa yameangushwa na Marekani katika miji ya Hiroshima na Nagasaki miaka kumi na mitano awali.

Bomu hilo lilifahamika kwa majina mengi sana kiufundi – kuna walioliita Project 27000, Product Code 202, RDS-220, na Kuzinka Mat (Mamake Kuzka).

Lakini sasa hufahamika zaidi kama Tsar Bomba – ‘Bomu la Tsar’.

Tsar Bomba halikuwa bomu la kawaida la nyuklia.