Mourinho: Najihisi dhaifu bila Fellaini Manchester United

Meneja wa Manchester United Jose Mourinho amesema anajihisi “dhaifu kiasi” bila Marouane Fellaini katika kikosi chake baada yake kuthibitisha kwamba mchezaji huyo wa safu ya kati huenda akakosa mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Kundi A dhidi ya FC Basel Jumanne.

Fellaini alikosa mechi ambayo walitoka sare ya 2-2 Jumamosi dhidi ya Stoke Ligi ya Premia kutokana na jeraha kwenye misuli ya sehemu ya chini ya mguu.

Mchezaji huyo wa taifa wa Ubelgiji amekuwa akipendwa na pia kuchukiwa na mashabiki tangu alipojiunga na klabu hiyo mwaka 2013.

Lakini Mourinho amesisitisa thamani yake.

“Namhitaji,” amesema.

“Ni mchezaji muhimu sana kwangu, muhimu zaidi kuliko mnavyoweza kufikiria. Najihisi dhaifu bila yeye.”

Phil Jones na Eric Bailly pia watakosa mechi hiyo kwani wanatumikia marufuku ya Uefa.

Hii ina maana kwamba Chris Smalling na Victor Lindelof wataanza katika safu ya ulinzi.

Mourinho pia amethibtisha kwamba David de Gea atakuwa langoni badala ya Sergio Romero, ambaye alichezeshwa katika michuano ya vikombe msimu uliopita.

Manchester United wamerejea Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu 2015 baada ya kushinda Europa League msimu uliopita.

Pamoja na Basel, United wamo kwenye kundi moja na Benfica na CSKA Moscow.